...

4 views

Alipokataa kurudi nyumbani
Alipokataa kurudi nyumbani...

NIMESHAPATA
Njiwa peleka ujumbe,kwa yule wangu muhibu
Aleninywesha kikombe,cha dhiki na masaibu
Na akaniacha hambe,sina kitu ela tabu
Mwambie nimeshapata,aridhiye moyo wangu

Usiseme kwa vijembe,mambo ukayaharibu
Na wala usimchimbe,japo ni msi adabu
Sema naye ka mjumbe,mwingi wa ustarabu
Mwambie nimeshapata, ambaye ni kufu yangu

Mwambie sina uvimbe,na vilema vya aibu
Hivi sasa ni kiumbe,kipya na nina tabibu
Amenitibu kwa tembe,za neni nzuri na hibu
Mwambie nimeshapata,tabibu wa moyo wangu

Msemeze ja kikembe,ili asione tabu
Kuuelewa ujumbe,akajiona ni dubu
Na ingabidi ufumbe,fanya hivyo taratibu
Mwambie nimeshapata, kijito cha raha yangu

Mwambie jino la pembe,limenifaa ajabu
Lishaziba pengo kumbe,limekuwa mjarabu
Nimeridhi linipambe,wajihi kama dhahabu
Mwambie nimeshapata,aliyeumbwa wa kwangu

Sir Ken Stan
© Ken Stanley