...

3 views

SIKUACHI MUHIBATI.
SIKUACHI MUHIBATI
Ewe wangu wa moyoni,nimpendaye kwa dhati
Hani wangu wa zamani,sasa na kila wakati
Wasiwasi ni wa nini,kihoro na atiati?
Sikuachi habitati,nikakutia huzuni

Sikuachi habitati,nilishakula yamini
Kwamba mwengine sifati,nikakuacha mwandani
Basi chani kibuhuti,kikunyimacho amani!
Daima ni wako hani,na mwengine sitafuti

Daima ni wako hani, kukupenda ni shuruti
Hufutiki akilini,na milele sikufuti
Basi hofu ni ya nini,kiasi raha hupati?
Kamwe sitokusaliti,nikakutia dhikini

Kamwe sitokusaliti,kufata kina fulani
Wanganita switihati,au kunipa vipeni
Bure hawana bahati,wewe ndiwe wa moyoni
Naja hivi karibuni, sikawii naja shoti.

Naja hivi karibuni,naja wawili tuketi
Tumwage yalo moyoni,na tupange mikakati
Ya kuishi kwa amani,kwa huba zilo thabiti
Naja hima muhibati,naja karibuni hani


© Ken Thuranira